AHAS GROUP Wachangia Kuimarisha Sekta Ya Elimu Zanzibar

  • Jan 25, 2018
  • 159 Views

Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimatifa na Uratibu wa Wazanzibari wanaoishi Nchi za Nje Ndg. Adila Hilal Vuai ameutaka Uongozi wa Skuli ya Jang’ombe Msingi “B” kuvitumia vyema vifaa vilivyotolewa na Jumuiya ya AHAS GROUP kupitia Bwana Ali Talib ambae ni mmoja kati Wazanzibari wanaoishi Nchi za Nje aliyeitikia wito wa Mhe. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt Ali Mohammed Shein ya kuwatambua, kuwashahisha na kuwashirikisha wazanzibari wanaoishi Nje ya Nchi kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya nchi yao. 

Alisema vifaa hivyo vinahitaji kulindwa na kutunzwa ili viweze kutumika kwa muda mrefu na kufanikisha lengo la Serikali la kuimarisha utoaji wa elimu bora kwa wananchi wake. Bi Adila, ameyaeleza hayo alipokuwa akizungumza na Uongozi wa Kamati ya Skuli ya Jang’ombe Msingi “B” mara baada ya kukabidhi vifaa vya elimu kama meza, viti, Computer na vyenginevyo kutoka kwa AHAS GROUP.

Akipokea vifaa hivyo kwa niaba ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, muakilishi wa Idara ya Elimu, Maandalizi na Msingi Bi Asia Hassan Mussa ameipongeza jumuiya hiyo kwa kuwa na moyo wa kutoa kwa upendo na kusaidia vifaa hivyo, ambavyo vitahuisha mkakati wa Wizara katika ukuzaji na uimarishaji wa utoaji wa elimu Zanzibar. 

Nae muakilishi wa AHAS GROUP Bwana Ali Talib amesema wataendelea kutoa misaada ya namna hiyo kila hali itakaporuhusu.  Toka kuanzishwa kwa kitengo cha Uratibu wa Wanadiaspora hapa Zanzibar, wanadiaspora wamekuwa mstari wa mbele kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuchangia katika sekta za afya na elimu.

Mkurugenzi Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa na Uratibu wa Wazanzibar wanaoishi nje ya nchi akiwa na mwakilishi wa AHAS GROUP.
Mkurugenzi Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa na Uratibu wa Wazanzibar wanaoishi nje ya nchi akiwa na mwakilishi wa AHAS GROUP.

Related Articles